SIMULIZI
inazidi kunoga. JB anaendelea kueleza kila kitu alichopitia maishani
mwake, sasa yuko katika kipengele cha safari yake ya sanaa. Tangu wakati
wa maigizo hadi sasa kwenye filamu, ambako anaendelea kutengeneza pesa
kupitia kazi hiyo ya uigizaji.
Wiki iliyopita, alieleza jinsi
alivyoanzisha kampuni ya kuzalisha filamu ya Jerusalem. Akieleza pia
ugumu aliokutana nao. Je, nini kilifuata?
TWENDE PAMOJA…
“Kwa hiyo nikabaki peke
yangu kwenye kampuni, sikukata tamaa, nikajipa moyo na kuendelea kukaza
buti,” anasema JB kwa msisitizo zaidi.
“Unajua filamu ya Kanisa la Leo,
ilichelewa sana kuingia sokoni, kwa hiyo nikawa nimetengeneza filamu ya
Agano la Urithi, ambayo iliingia sokoni kabla ya ile ya mwanzo,”
anasema.
“Wakati naendelea kuwaza, nikaamua
nimuite Richie ili tuwe pamoja kwenye kampuni yangu, nikaanza
kumshawishi, nikamshawishi aachane na kazi yake kwenye kiwanda cha Chai
Bora, kwa kuwa Richie anapenda sana kuigiza, aliamua kuacha kazi na kuja
kuungana na mimi kwenye kampuni yangu ya Jerusalem,” anabainisha JB.
“Nikamfanya kuwa partner, yaani
tukagawana hisa kwenye hiyo kampuni, tukatengeneza filamu ya Stranger,
filamu ambayo hakika sitaisahau katika maisha yangu ya uigizaji,”
anasema JB huku akijirekebisha vyema kwenye kiti.
“Kwa nini kaka,” najikuta nikimtupia swali huku nami nikiirekebisha vyema tai yangu.
“Ilikuwa ni filamu ya kwanza kunipa tuzo
kama Muigizaji Bora wa Kiume, hakika sinema hiyo ilinipa morali na
bidii zaidi katika kufanya kazi yangu ya uigizaji,” anasema JB na
kunitazama usoni kwa muda kabla hajaendelea.
“Basi, heshima ikaanza kujengeka tena,
lakini kwa wakati huo, mtu aliyekuwa akiheshimika zaidi kwenye tasnia ya
filamu ni Gabriel Mtitu wa Game First Quality Tz Limited, akiwa na
wasanii wakubwa kama Ray na Kanumba, hakika alikuwa ameliteka sana
soko,” anasema.
“Ngoja niwe mkweli katika hili pia,
huwezi kutaja orodha ya watu waliochangia kuinua sanaa ya uigizaji
nchini, usimtaje Mtitu wa Game, huwezi, wapo wengi kama Sultan Tamba,
Musa Banzi, hawa ni watu ambao wana mchango mkubwa sana kwenye ukuaji na
upanukaji wa sanaa ya uigizaji hapa nchini,” anasema JB bila kupumzika.
“Kwa hiyo, ushindani ulikuwepo mkubwa,
lakini pamoja na hayo, mimi na Richie tuliendelea kujipa moyo kuwa,
lazima tufike mbali kwa kazi hii ya sanaa,” anasema.
Kwa wakati huo, tulikuwa tukisambaza
sinema zetu na Kampuni ya Mwananchi Store, chini ya msambazaji Farhaji
Mohamed,” anasema JB.
“Kwa hiyo, kazi zikaendelea kufanyika,
tukaigiza sinema moja ya Swahiba, ambayo kwa hakika kabisa ilitupa jina
kubwa sana kwenye tasnia ya filamu hapa nchini, ni filamu ambayo
iliongeza heshima kwenye kampuni yetu,” anasema JB.
“Kuna kitu nataka kusahau, unajua watu
wengi hudhani nimeanza kuigiza na Mzee Majuto kwenye filamu za Shikamoo
Mzee na Nakwenda kwa Mwanangu, la hasha, mzee huyu niliwahi kuigiza
naye sinema moja huko nyuma, lakini haikujulikana sana, iliitwa
Pwaguzi,” anasema JB na kusindikiza maelezo hayo kwa kicheko cha juu.
“Pia, filamu ya Swahiba, ndiyo
iliyomtambulisha kwenye ramani ya uigizaji msanii mmoja mkali sana wa
kike hapa Bongo, si mwingine bali ni Rose Ndauka, tulikutana naye huko
kwao maeneo ya Kigogo, tukaamini anaweza kuigiza, tukampa mafunzo na
kuigiza naye sinema hiyo,” anasema.
“Hata hivyo, mwishoni mwa mwaka 2007
kama sikosei, Richie aliniambia, kutokana na ukuaji wa sanaa kwa wakati
huo, ni bora naye ajitegemee kwa kuanzisha kampuni yake ya kuzalisha
filamu, niliumia sana, maana nilikuwa nimemzoea sana Richie, lakini
sikuwa na jinsi,” anasema.
“Richie akaanzisha Kampuni ya Bulls,
ambayo filamu ya kwanza kuigiza iliitwa Mahabuba, alinishirikisha pia,
tulifanya kwa moyo wote kabisa na maisha yakaendelea,” anasema.
“Nikaendelea na kuzalisha filamu,
nikaamua kuungana tena na msanii nguli ambaye kwa sasa ni marehemu, Adam
Kuambiana, ambapo nilimuajiri kama muongozaji wa filamu za kampuni
yangu,” anasema JB.
Je, nini kitafuata? Usikose wiki ijayo