Siku
zote najua kila mtu anapenda kuwa na mtu ampendaye. Najua fika hata
wewe unayesoma hapa unatamani mpenzi wako akupende kama unavyompenda
wewe ikiwezekana yeye azidishe mapenzi.
Hicho si kitu kibaya kwani najua raha ya
kupendwa. Lakini sasa wakati hali ikiwa hivyo huwa nawashangaa sana
wale wanawake ambao wanafikia hatua ya kutumia pesa zao nyingi kwenda
kwa waganga eti ili waume au wapenzi wao wawapende, wawanyenyekee, hivi
huu ni uungwana kweli?
Yaani mwanamke na akili zake,
anadunduliza pesa kisha badala ya kuzifanyia mambo ya msingi anakwenda
kwa sangoma eti ili akamzubaishe mume asifikirie wanawake wengine zaidi
yake, ni uungwana?
Mimi sikatai kwamba kila mmoja lazima
afanye awezalo kuhakikisha anamshika vilivyo mtu wake lakini sidhani
kwamba kumuendea mumeo kwa mganga ni jambo la busara.
Mbaya zaidi wengine huenda huko kisha
kuomba wapewe dawa za kuwapumbuza waume zao, eti kila anachotaka apewe,
akisema lolote asikilizwe, akimwambia mume leo hakuna kwenda kazini,
mume akubali, aah kweli umgeuze mumeo awe zezeta kiasi hicho! Maisha
gani hayo?
Kama umeshindwa kutumia njia sahihi za
kumshika huyo mume wako heri umuache akatafute mwingine na wewe uchukue
hamsini zako lakini siyo kwenda kununua limbwata la kulazimisha mambo
yasiyoleta picha nzuri kwenye jamii.
Wakati mwingine inasikitisha sana,
unakuta mwanaume kwenye familia yake hana sauti kabisa, kila kitu
anachosema mke yeye hewala. Mke akitaka kwenda kwenye mambo yake, hata
asipoaga, asiulizwe na kweli mume ananyamaza.
Mume akipokea mshahara wake, moja kwa
moja kwa mkewe, eti mke ndiye anaupangia bajeti huku akijisevia za kwake
za kufanyia mambo yake.
Ndugu au wazazi wa mume wakihitaji
msaada wa fedha, mke huzuia wasipewe na mwanaume husika hukubali kwa
kuhofia kumpinga mkewe atakuwa kamkosea sana.
Mwanamke kumfanyia hivyo mumewe hakuna
ubaya, ambapo huwajali wazazi na ndugu zake ambao wakiomba msaada wowote
hutekelezewa ‘fasta.’
Mume anapangiwa ratiba ya kufanya kazi za ndani, hee jamani! Hayo ndiyo mahaba kweli au kudhalilishana?
Hivi mumeo akiwa zezeta wewe unasikia
raha gani? Kwamba wewe sasa uwe ndiye mwenye sauti, ukisema mume
ananywea! Noh! Hii siyo sawa na wanawake mnaifanya hivyo mnakosea na
siyo uungwana